Halmashauri ya Manispaa ya Singida leo Oktoba 6, 2025 imepokea madaktari bingwa mbalimbali kupitia mpango wa Madaktari Bingwa wa Mama Samia, ambao wataanza kutoa huduma kwa muda wa siku tano katika Hospitali ya Manispaa hiyo.
Madaktari hao bingwa ni pamoja na bingwa wa magonjwa ya wanawake na ukunga, bingwa wa watoto na watoto wachanga, bingwa wa upasuaji, bingwa wa usingizi na ganzi, bingwa wa magonjwa ya ndani, bingwa wa kinywa na meno pamoja na muuguzi mbobezi.
Akizungumza wakati wa mapokezi yao, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Singida alisema ujio wa madaktari hao ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa manispaa hiyo ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo.
“Huduma hizi ni fursa adhimu kwa wananchi wa Singida. Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupata matibabu, hasa wale waliokuwa wakikumbwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za kibingwa,” alisema.
Mpango huu wa Madaktari Bingwa wa Mama Samia umeendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya za kibingwa, hasa katika maeneo ya pembezoni na yenye upungufu wa watalaam.
Huduma hizo zinatarajiwa kutolewa kuanzia leo hadi Oktoba 10, 2025, katika Hospitali ya Manispaa ya Singida. Wananchi wametakiwa kufika hospitalini mapema ili kupata huduma kulingana na mahitaji yao ya kiafya.